Government of Saskatchewan
Quick Search:
Tuesday, May 24, 2016

 Yaliyomo

1. Kuwasili
2. Aina za Nyumba
3. Kupanga Nyumba
4. Kununua Nyumba
5. Mipango ya Msaada wa Nyumba
6. Huduma za Kinyumbani

1. Kuwasili

Swali: Nitakaa wapi nikiwasili?

Watu wengi waliofika hivi karibuni hukaa hotelini wanapowasili mara ya kwanza. Hakikisha kwamba umefahamisha hoteli kimbele ili waweze kuhifadhi nafasi.  Njia moja ya kupata habari kuhusu hoteli ni kutumia intaneti au Kurasa za Njano (Yellow Pages) za kitabu cha simu cha Saskatchewan. Unaweza pia kutafuta  vitabu vya simu  (phone books) vya Saskatchewan kwenye intaneti.

Unaweza kuwasiliana na hoteli ili kupata malipo na huduma zao. Kwa mfano, baadhi ya hoteli zina jikoni zilizo na vyombo vya upishi, basi unaweza kujipikia. Pengine utapenda kupata makao yaliyo karibu katikati ya jiji ambapo itakuwa rahisi kutuma maombi ya kupata stakabadhi muhimu na kuchukua hatua nyingine za kwanza-kwanza za kukaa Saskatchewan.

Kama tayari umewasili Saskatchewan, wasiliana na ofisi iliyo karibu ya Kituo cha Kanda cha Wahamiaji Wapya (Regional Newcomer Gateway) ili kuona kama watakupendekezea makao ya muda ya kuishi.

Swali: Ninahitaji kujua nini kuhusu kukodisha hoteli?

Mara nyingi utahitaji kadi ya benki ili kuhifadhi vyumba mapema. Kama huna kadi ya benki nawe umekuja hapa kufanya kazi, mwajiri wako anaweza kukusaidia.

Wenye hoteli watakuambia saa ya kuingia humo (huu ni wakati ambao chumba chako kitakuwa tayari) nao watakuambia saa ya kuondoka (huu ni wakati ambao ni lazima uondoke kwenye chumba chako). Ukiendelea kukaa chumbani mwako baada ya saa ya kuondoka kwisha, huenda ukatozwa malipo ya usiku mwingine.

Baadhi ya hoteli hukodisha vyumba kwa wiki nzima badala ya siku moja-moja. Huenda malipo ya kukodi kwa wiki nzima yakawa nafuu kuliko ya siku moja-moja.

Swali: Ninawezaje kusafiri kutoka uwanja wa ndege hadi kwenye makao yangu?

Majiji mkoani Saskatchewan yana huduma za teksi lakini kwa habari ya jumuia ndogo-ndogo, miji na vijiji vidogo mara nyingi havina. Viwanja vya ndege viwili vikuu vya Saskatchewan vilivyo katika Regina na Saskatoon vina vituo vya teksi nje kidogo ya uwanja wa ndege, na simu za moja kwa moja ndani ya uwanja wa ndege za kuita teksi.

Malipo ya teksi Saskatchewan yameshawekwa mapema kwa hiyo hakuna haja ya kupiga bei na dereva. Safari kutoka uwanja wa ndege wa Regina hadi maeneo ya katikati ya jiji hugharimu takriban dola 10.00 hadi 20.00. Safari kutoka uwanja wa ndege wa Saskatoon hadi maeneo ya katikati ya jiji hugharimu takriban dola 15.00 hadi 25.00. Kama familia yako ni kubwa, au kama una mizigo mingi, unaweza kuita basi dogo, lakini hilo litagharimu kuliko gari dogo.

Kama unaenda kwenye makao yaliyo nje ya Regina au Saskatoon, utahitaji kufanya mipango ya kupanda basi au umwombe mtu akuchukue kwenye uwanja wa ndege.

Kama umekuja kufanya kazi, huenda mwajiri wako akakusaidia kupata usafiri kutoka uwanja wa ndege hadi mahali utakapokaa unapowasili kwa mara ya kwanza. Huenda pia mwajiri wako akakusaidia kupata usafiri kwenda mahali utakapokuwa ukifanya kazi.

Swali: Nitanunua wapi vitu muhimu, kama chakula na kadi za simu, baada ya kuwasili?

Kuna sehemu mbalimbali. Kuna mikahawa inayoandaa chakula kwa bei mbalimbali, lakini kwa kawaida ni nafuu kujipikia mwenyewe. Ili kupata chakula cha kupika, au chakula tayari (kwa mfano, sandwichi, saladi, na nyama iliyopikwa) tafuta duka la vyakula.

Katika vituo vikubwa, kuna maduka makubwa yanayouza bidhaa zote unazohitaji zikiwemo chakula, nguo, fenicha, vifaa vya matumizi ya binafsi (kwa mfano, sabuni na karatasi za choo), na kadi za simu.

Katika mitaa mingi, maduka madogo na maduka ya dawa huuza bidhaa za vyakula, kadi za simu, na vifaa vya binafsi. Maduka hayo kwa kawaida yanakuwa ghali kuliko maduka ya vyakula na maduka makubwa.

Wakati unanunua kadi ya simu, uliza kama inatoa huduma kwenda katika nchi unakohitaji kupiga simu.

2. Aina za Nyumba

Swali: Ninaweza kupata nyumba za aina gani katika Saskatchewan?

Katika Saskatchewan unaweza kupanga au kununua nyumba. Kuna mambo mengi unayohitaji kujua kuhusu kupanga au kununua nyumba. Kwa mfano, utahitaji kujua kwamba kupanga na kununua nyumba ni mapatano ya kisheria.

Tovuti ya Nyumba kwa Wahamiaji Wapya (Housing for Newcomers) ina habari kuhusu kupanga, kununua na kudumisha nyumba yako. Tovuti hiyo pamoja na machapisho yaliyomo yanapatikana katika lugha mbalimbali. Moja ya machapisho ni Mwongozo wa Mhamiaji Mpya Kuhusu Nyumba za Kanada (The Newcomer’s Guide to Canadian Housing). Chapisho hilo hutoa habari za msingi kuhusu nyumba za Kanada, madokezo mafupi ya kupata nyumba za kupanga, na hueleza maneno hususa yanayotumiwa katika kununua na kupanga.

 

Chapisho la Shirika la Kisheria la Elimu ya Umma la Saskatchewan (SKEU) (Public Legal Education Association of Saskatchewan (PLEA))huandaa habari za kisheria kuhusu kupanga au kununua nyumba.

3. Kupanga Nyumba

Swali: Nitapataje nyumba ya kupanga mkoani Saskatchewan?

Nyumba nyingi za kupanga katika Saskatchewan zinamilikiwa na watu binafsi au makampuni, wala si serikali.

Kuna aina nyingi za nyumba za kupanga, zikiwemo:

 • Fleti (Apartments) (hizi ndizo nyumba zinazotumiwa na wapangaji wengi zaidi)
 • Nyumba (Houses) (nyakati nyingine huitwa nyumba za familia moja-moja)
 • Nyumba za mjini (Townhouses)
 • Kondominiamu (Condominiums) (hizi ni fleti zinazomilikiwa na watu binafsi.
 • Ukipanga nyumba ya aina hii, kwa ujumla unaipanga kutoka kwa mtu binafsi badala ya kampuni)

Chumba kimoja katika nyumba ambazo jikoni na bafu hutumiwa kwa pamoja Ili kupata makao ya kupanga, unaweza:

 • Kutafuta kwenye intaneti tovuti zinazohusu kupanga nyumba.
 • Tazama matangazo katika magazeti ya Saskatchewan, hasa katika safu ya matangazo mafupi ya Kupangisha (For Rent).   Unaweza kuona matangazo ya magazeti ukitumia tovuti zao.  Weka gazeti (“newspaper”) na jina la mji.
 • Piga simu kwenye ofisi iliyo karibu ya Kituo cha Kanda cha Wahamiaji Wapya (Regional Newcomer Gateway) ili kupata ushauri kuhusu kupata nyumba za kupanga katika eneo lako.
 • Angalia mabango ya Kupangisha (For Rent), yaliyobandikwa nje ya fleti na nyumba.

Swali: Nitachaguaje nyumba nzuri ya kupanga?

Maswali yafuatayo yanaweza kukusaidia kuamua kama umepata nyumba nzuri ya kupanga.

 • Je, hali ya mahali hapo ina hatari zozote za kiafya au za kiusalama? Kwa mfano, je, kuna kuvu, wadudu au panya? Je, kuna umeme, maji ya bomba, na mfumo wa kupasha joto? Mmiliki wa nyumba (mtu anayetaka kukupangisha nyumba) anahitajika na sheria kuhakikisha kuwa jengo hilo ni salama na safi.
 • Je, kuna nafasi ya kutosha kwa watu watakaoishi humo? Huenda mmiliki akaruhusu tu idadi hususa ya watu kuishi katika nyumba hiyo.
 • Malipo ni pesa ngapi na malipo hayo ya kupanga yanatia ndani mambo yapi? Kwa mfano, je, yanajumuisha gharama za maji, mfumo wa kupasha joto, na umeme?
 • Amana ya usalama ni pesa ngapi? Amana ya usalama (safari nyingine huitwa amana ya uharibifu) ni pesa unazomlipa mmiliki wa nyumba, ikiwa itatukia kwamba umeharibu nyumba, umeshindwa kulipa kodi ya kupanga, au ikiwa usafi unahitajika baada yako kuhama. Mara nyingi hiyo hutozwa mwanzoni mwa kupanga nyumba. Kiasi cha juu zaidi ambacho mmiliki wa nyumba anaweza kukutoza kuwa kama amana ya usalama ni kodi ya kupanga ya mwezi mmoja. Utarudishiwa wakati wa kuhama.
 • Je, nyumba hiyo hupangwa kwa msingi wa mwezi kwa mwezi au je, utahitajika kusaini mkataba wa kupangisha wa muda mrefu? Mkataba wa kupangisha ni mapatano yanayoorodhesha haki na majukumu ya kila mmoja (mmiliki na mpangaji) kwa muda fulani. Hiyo inamaanisha kuwa umeweka mapatano ya kuishi hapo kwa muda ambao mkataba wako wa kupangisha husema (kwa mfano, mikataba ya kupangisha mara nyingi ni mapatano ya mwaka mmoja). Soma mapatano hayo kwa makini na utafute msaada kama huelewi jambo fulani. Utahitajika kutoa taarifa ya mapema unapotaka kuhama na huenda ukatozwa malipo fulani kama utahama kabla ya kukamilika kwa mkataba wako.
 • Je, ni mahali panapopendeza – palipo karibu na mahitaji yako kama vile mahali pa kazi, shule, barabara ya basi, au duka la vyakula?
 • Je, inaruhusiwa kufuga wanyama vipenzi? Katika Saskatchewan, nyumba nyingi za kupanga haziwaruhusu wapangaji kufuga wanyama, kwa hiyo kama una mnyama kipenzi ni muhimu kuuliza swali hilo.

Haya ni baadhi ya madokezo muhimu kuhusu kupanga nyumba:

 • Kabla ya kupanga, kagua makao hayo vema. Mmiliki wa nyumba akikosa kukupa daftari la kuandikia unapokagua makao hayo, tumia Daftari la Uchanganuzi wa Nyumba ya Kupanga (Rental Unit Evaluation Worksheet).
 • Kutumia daftari hilo kunaweza kukusaidia kuamua kama nyumba hiyo ni salama, starehe, na kufaa mahitaji yako. Orodhesha vitu vyote ambavyo havifanyi kazi au vinavyohitaji kurekebishwa. Usipotia alama sehemu zilizoharibika kwenye daftari, huenda mmiliki wa nyumba akadhani wewe ndiwe uliyefanya uharibifu huo. Kwa hiyo, wakati utakapohama, amana yako yote, au sehemu yake, itatumiwa kufanya marekebisho hayo. Basi ni muhimu kukagua kwa makini nyumba yako unapoingia. 
 • Wamiliki wengi wa nyumba huuliza kuhusu tabia na marejeo ya kifedha kutoka kwa wale wanaotaka kupanga nyumba. Huenda watu wa familia, marafiki au mwajiri wako akawa tayari kukupa marejeo hayo. Ofisi iliyo karibu ya Kituo cha Kanda cha Wahamiaji Wapya (Regional Newcomer Gateway) inaweza kukupendekezea njia nyinginezo.
 • Pata risiti (uthibitisho wa maandishi) kuwa umelipa amana ya usalama, na pia pata risiti za kawaida kwa ajili ya malipo yako ya kila mwezi ya kupanga.

Ili kupata habari kuhusu nyumba za kukodi  Saskatchewan, tembelea tovuti (Canada Mortgage and Housing Corporation (CMHC) website).

Swali: Mpangaji na mmiliki wa nyumba wana majukumu gani?

Unapopanga makao, inamaanisha kwamba wewe, mpangaji, unaingia katika mkataba wa kisheria wa upangaji na mmiliki wa nyumba hiyo.

Majukumu ya mpangaji ni pamoja na:

 • Kulipa kodi kwa wakati, mara nyingi hulipwa mwanzoni mwa kila mwezi, au kulingana na mkataba wako hususa wa kupangisha.
 • Kudumisha usafi wa makao yako, ikiwemo kuweka takataka kwenye pipa la takataka lililoandaliwa.
 • Kuheshimu sheria za jengo na haki za wapangaji wengine. Kwa mfano, kiasi cha kelele, maegesho ya magari, au maeneo yanayotumiwa kwa pamoja kama vyumba vya kufulia nguo.
 • Kutoa taarifa ifaayo unapotaka kuhama, kulingana na mkataba wako wa kupangisha. Taarifa lazima itolewe kwa maandishi, wala si kwa kumwambia tu mmiliki wa nyumba. Wizara ya Sheria ya Saskatchewan huandaa taarifa kielelezo (sample).

Majukumu ya mmiliki wa nyumba ni pamoja na:

 • Kuhakikisha kuwa jengo ni salama kuishi ndani
 • Kudumisha vifaa vyote katika hali ya kutenda kazi
 • Kufanya marekebisho yanapohitajika
 • Kuheshimu haki yako ya kutoingiliwa

Mmiliki ya nyumba anaweza tu kuingia kwenye makao yako kwa kukuomba ruhusa mapema, katika hali ya dharura, au wewe ukimpa ruhusa ya kuingia. Pia kuna sheria kuhusu ni jinsi gani na ni mara ngapi mmiliki anaweza kupandisha kodi na wakati anapopaswa kukujulisha kuhusu ongezeko la kodi ya kupanga.

Swali: Itakuwaje kama mimi na mmiliki wa nyumba tuna tatizo kati yetu tusiloweza  kutatua?

Inakupasa kushirikiana na mmiliki wa nyumba kupata suluhisho matatizo yanapotokea. Kama tatizo haliwezi kusuluhishwa, wasiliana na Ofisi ya Wapangaji wa Nyumba za Makao (Office of Residential Tenancies). Watu waliopo hapo wanaweza kusaidia kufafanua kinachotakiwa kwa wapangaji na wamiliki, na wanaweza kusaidia kusuluhisha ubishi.

Ofisi ya Wapangaji wa Nyumba za Makao hutoa huduma bila malipo.  Ikiwa unataka Mmiliki aweze kulipa pesa fulani, unapaswa kujaza fomu na kulipa ada ya dola 50.  Ikiwa wewe hutegemezwa na serikali (Social Assistance) haupaswi kulipa ada hii.

Ofisi Za Wapangaji wa Nyumba za Makao
(Office of Residential Tenancies)

Ofisi ya Regina
120-2151 Scarth St.
Regina SKS4P 2H8
ORT@gov.sk.ca

Ofisi ya Saskatoon
Main Floor,Sturdy Stone Building
122-3rd Avenue North
Saskatoon SK S7K @H6
ORT@gov.sk.ca

Wanaopiga Simu Bila Malipo: 1-888-215-2222
Wanaopiga Simu Kutoka Nje ya Saskatchewan:1-306-787-2699
Fax Bila Malipo:1-888-867-7776
Fax Kutoka Nje ya Mkoa:1-306-787-5574

4. Kununua Nyumba

Swali: Nitapata wapi habari kuhusu kununua nyumba?

Chapisho la Kununua Nyumba ya Kwanza Nchini Kanada; Mambo Wanayopaswa Kujua Wahamiaji Wapya (Buying Your First Home in Canada: What Newcomers Need to Know) hutoa habari muhimu kwa wahamiaji wanaotafuta kununua nyumba. Ili kupata habari kuhusu soko la ununuzi wa n ”yumba Saskatchewan, tembelea tovuti (Canada Mortgage and Housing Corporation (CMHC) website)

Swali: Nyumba za kuuzwa ni za aina gani?

Kuna aina mbalimbali za nyumba zinazouzwa kutia ndani zile ziitwazo condominiums, townhouses, detached homes (nyakati nyingine huitwa nyumba za familia moja¬moja), semi-detached homes, na duplexes.

Kwa ufafanuzi kuhusu kila moja ya nyumba hizo na kwa habari zaidi, tafadhali soma chapisho Kununua Nyumba ya Kwanza Nchini Kanada; Mambo Wanayopaswa Kujua Wahamiaji Wapya (Buying Your First Home in Canada: What Newcomers Need to Know).

Swali: Kununua na kumiliki nyumba huhusisha gharama zipi?

Ni muhimu kujua gharama hususa ya kununua na kumiliki nyumba. Bei za nyumba hutofautiana kulingana na ukubwa, hali, sura, na mahali zilipo. Utahitaji kuzingatia bei ya nyumba na ardhi na gharama nyingine kama vile kodi za kumiliki ardhi, ada za kisheria, kodi za kubadilisha umiliki wa ardhi, gharama za mkopo wa ujenzi (kutia ndani viwango vya riba) ada ya nyumba aina ya condominium (kwa ajili ya nyumba za condominium pekee), bima, huduma za kinyumbani, gharama za kuhama (kutia ndani fenicha utakazonunua), na gharama za marekebisho kama yatahitajika.

Ukitaka kufanya marekebisho makubwa kwenye nyumba (kama vile kuongeza vyumba katika nyumba), utahitaji kupata kibali cha ujenzi kutoka kwenye ofisi ya manispaa na kuna sheria kuhusu mabadiliko yatakayokubaliwa.

Ukiwa mmiliki wa nyumba, utahitajika kulipa kodi ya ardhi kwa ajili ya nyumba yako kila mwaka, kiasi ambacho hutofautiana kulingana na aina ya nyumba yako na eneo na ukubwa wa ardhi yenye nyumba yako. Pia una jukumu la kudumisha nyumba na ardhi yako.

Ikiwa utanunua nyumba aina ya condominium, utakuwa na jukumu tu la ndani ya nyumba yako. Ukiishi kwenye nyumba ya condominium, utalipa ada ya condominium. Ada hizo hutumiwa na kampuni kwa kusudi la kutunza uwanja ulio nje ya nyumba na kutunza sehemu za ardhi zinazotumiwa kwa pamoja (kama vile maegesho ya magari). Ada za condominium za majengo mbalimbali huenda zikatumiwa kutimiza mambo mbalimbali, kwa hiyo hakikisha umeuliza jinsi ada yako itakavyotumiwa.

Swali: Nitapata wapi nyumba ya kununua?

Unaweza kununua nyumba kupitia mawakala wa ardhi au moja kwa moja kutoka kwa mmiliki wa nyumba.

Ili kupata nyumba ya kununua:

 • Tazama nyumba (ardhi) zinazouzwa kwenye magazeti ya eneo lako (safu ya matangazo mafupi ya kibiashara), hasa katika magazeti ya mwisho wa wiki, na kwenye tovuti za mambo ya kununua nyumba.
 • Wasiliana na wakala wa mauzo ya ardhi wa eneo lako. Mawakala wa mauzo ya ardhi hulipwa kwa kazi yao na mtu anayeuza nyumba, basi si lazima uwalipe ili wakusaidie kununua nyumba. Unaweza kupata orodha ya kampuni za mauzo ya ardhi katika Kurasa za Njano (Yellow Pages) katika vitabu vya simu vya eneo lako au kupitia Shirika la Wauzaji Ardhi Saskatchewan (Saskatchewan Realtors) kwenye intaneti. 
 • Tembelea mitaa mbalimbali ambapo utapenda kuishi na utazame mabango yaliyoandikwa Inauzwa (For Sale), kisha wasiliana na muuzaji.

Swali: Nitafanya nini wakati nimepata nyumba ninayopenda kununua?

Utahitaji kumwambia mmiliki bei unayotaka kulipa (katika maandishi), utaje amana unayotaka kuwekea nyumba hiyo, ufanye mipango ya ukaguzi wa nyumba, na upate mkopo wa nyumba kutoka benki. Wakala wa mauzo ya ardhi au wakili anaweza kukusaidia kuhusiana na utaratibu huo.

5. Mipango ya Msaada wa Nyumba

Swali: Nitapataje msaada wa gharama za nyumba?

Saskatchewan Housing Corporation Programs and Services

Shirika la (Saskatchewan Rental Housing Supplement (SRHS)) husaidia familia zenye watoto au watu walemavu kulipa kodi

Swali: Je, kuna punguzo la kodi kwa watu wanaonunua nyumba kwa mara ya kwanza?

Ndiyo. Punguzo hilo linaitwa Punguzo la Kodi kwa Wanunuaji wa Nyumba (PKWN) (Home Buyers' Tax Credit (HBTC) nalo liko kwenye mpango wa mamlaka ya shirikisho.

6. Huduma za Kinyumbani

Swali: Huduma za kinyumbani ni nini?

Hizo ni huduma kama vile umeme, maji, maji-taka, simu, na gesi zinazotumiwa katika nyumba za Saskatchewan. Huduma hizo kwa kawaida huandaliwa kupitia shirika la serikali ya mkoa au ya manispaa, ila tu huduma za intaneti na simu za mkononi, ambazo pia huandaliwa na kampuni binafsi.

Swali: Nitafanye ndipo niletewe huduma za kinyumbani?

Ni lazima uwasiliane na mwenye kutoa huduma hizo. Utaratibu huo pia huitwa kupata upatanisho (hook-up). Unaweza kuwasiliana kupitia simu, kwa kutembelea ofisi husika au kutoa ombi la kuletewa huduma kupitia tovuti ya mwenye kutoa huduma hiyo. Kwa kawaida ada fulani hulipwa kwa ajili ya kuletewa huduma, nayo itaongezwa kwenye bili yako ya mwezi wa kwanza. Unaweza kulipa bili za huduma kupitia barua, au wewe binafsi kwenye ofisi ya mtoa-huduma, au kwenye mtandao.

Swali: Ni nani hutoa huduma hizo?

Gesi – Katika maeneo mengi ya Saskatchewan, gesi ndiyo hutumiwa kama kuni za kupikia. Shirika linatoa huduma za gesi katika mkoa linaitwa SaskEnergy. Unaweza kupata mahali zilipo ofisi zake kotekote Saskatchewan kwenye tovuti ya NishatiSask (SaskEnergy).

Umeme – Huo hutolewa na shirika la UmemeSask (SaskPower). Ili kupata habari zaidi kuhusu kupata au kukatiza huduma za umeme, tembelea tovuti ya UmemeSask (SaskPower).

Huduma ya maji na maji-taka – Jiji lako, mji au shirika lingine la serikali husimamia huduma hizi. Angalia simu ya shirika la maji na maji-taka katika sehemu ya jiji kwenye kitabu cha simu cha eneo lako au kwenye tovuti ya jiji lako. Kama unaishi katika mji au kijiji, huenda ikawa lazima kupiga simu kwenye ofisi ya Mji au Kijiji ili uletewe huduma hizo.

Intaneti na Simu – Kuna kampuni mbalimbali za intaneti, simu, na simu za mkononi zinazoweza kutoa huduma za kutimiza mahitaji yako. Unaweza kuzipata kwenye Kurasa za Njano (Yellow Pages) katika kitabu cha simu au kwenye mtandao kwa kutumia Kifaa cha Kutafuta cha Kitabu cha SimuSask (Sasktel Phonebook Search tool). Kwa mfano, andika maneno Kampuni za Simu (Telephone Companies) kando ya Aina (Category), andika jiji au mji unakoishi kando ya maneno Jiji/Mji (City/Town), kisha bonyeza Tafuta (Search).

Unapoingia kwenye mkataba wa kupata simu ya mkononi, ni muhimu kujua gharama zote zinazohusika, kutia ndani ada za huduma na ada za simu za kanda au za mbali baada ya kumaliza kutumia dakika za bure. Kampuni nyingi za simu za mkononi hutoza ada fulani kama unataka simu yako ikatizwe.

Swali: Je, maji ya bomba katika jumuia za Saskatchewan ni salama kunywa?

Sheria za Serikali ya Saskatchewan hutaka vyanzo vyote vya maji, vya umma na vya ushirikiano wa umma-binafsi, vipimwe ili kuhakikisha kuwa maji hayo ni salama kunywewa. Visima vya kibinafsi havitiwi kwenye sheria hizo.

Ikiwa una shaka kama maji yako ya bomba ni salama, tafadhali mpigie simu mwenye kutoa huduma zako za maji. Maduka huuza maji ya chupa, vichujio vya maji, na dawa za kusafisha maji. Unaweza kupata habari zaidi kuhusu kupima maji (hapa).© 2016 Government of Saskatchewan. All rights reserved.